WANASAYANSI na teknolojia wamepata njia mpya ya kupambana na magonjwa mapya nyemelezi

Share it:

MIAKA mitano iliyopita wanasayansi walivumbua njia ya kutengeneza chembe nyingi za msingi za mwili wa mwanadamu (human stem cells). Chembe hizo zinaweza kuendelea kukua vizuri na kuwa kama chembe nyingine yoyote kati ya chembe mbalimbali zisizopungua 200 zilizo katika mwili wa mwanadamu, ikiwa ni pamoja na chembe za kongosho. Anaandika WILLIAM SHAO.

WANASAYANSI na teknolojia wamepata njia mpya ya kupambana na magonjwa ambayo hapo awali hasingeweza kutibiwa kwa njia za kisasa za kutumia chembe za msingi. Lakini sasa ni jambo linalowezekana. Jarida maarufu, TIME tole la Mei 30, 2005, linasema maabara mbalimbali nchini Marekani zimetengeneza aina mbili za chembe za msingi ambazo ni 'chembe za kiinitete' na 'chembe za uzazi'.

Jarida hilo limeunga mkono jarida, New Scientist ambalo linasema: "Chembe za msingi huenda zikazalisha chembe mpya zinazoweza kufanya kazi ya zile chembe zilizoharibiwa na magonjwa mengi hatari." Baadhi ya magonjwa hayo ni ugonjwa wa kutetemeka, kisukari, maradhi sugu ya moyo, ugonjwa wa figo, kuharibika kwa ini na maradhi ya kansa.

Chembe hizo zinaweza kutengeneza damu pia, kitu ambacho kinaweza kusababisha benki za damu zifungwe. Zaidi ya hilo, madaktari wamekuwa wakitumia chembe hizo kwa miaka mingi kutibu ugonjwa wa damu.

Kwa kawaida, matibabu hayo ni pamoja na uboho wa mifupa ambao una chembe nyingi sana zinazotengeneza damu. Madaktari hupenda kukusanya chembe hizo kutoka katika damu iliyoko mwilini. Inatarajiwa kuwa na matibabu yanayotumia chembe za msingi ambayo yataweza kutengeneza tishu mpya za mwili.

Kama ilivyo katika jambo lolote jipya, mambo fulani katika sayansi hii mpya yamezusha mzozo. Watu wengi, ikiwa ni pamoja na baadhi ya wanasayansi, wanahisi kwamba kutumia chembe za msingi za mwili wa mwanadamu, na hasa chembe zinazotokana na viinitete au mimba changa, ni kutothamini uhai wa mwanadamu.

Sayansi hiyo inayoheshimiwa sana na watu, inapingwa na wengine baadhi. Kila uvumbuzi mpya kama huu unapotokea unazusha zogo. Wanaounga mkono matumizi ya chembe za msingi wanaamini kwamba hizo zitatibu magonjwa mengi zaidi na UKIMWI ukiwa mmojawapo.

Lakini chembe hizo ni nini? Zinapatikanaje? Ikiwa zina faida kama zinavyosemwa na kutabiriwa, kwanini suala hilo linazusha mzozo? Chembe za kiinitete zinaweza kutengeneza zaidi ya chembe 200 tofauti zilizo katika mwili wa mwanadamu. Jinsi gani zinatengenezwa, hilo ndilo swali la msingi.

"Mara tu baada ya mimba kutungwa," kinaandika kitabu cha Abortion, "chembe ya yai husika huanza kugawanyika". Chembe ya mwanadamu hugawanyika kwa kiasi cha siku tano na kutengeneza kibonge cha chembe. Kibonge hicho huwa na umbo la duara lenye tabaka la nje la chembe, kikundi kidogo chenye chembe kiasi kwa upande wa ndani.

Chembe hizo za ndani hung'ang'ania kwenye ukuta wa ndani wa duara hilo. Tabaka la nje hutengeneza kondo wa nyuma. Chembe zilizo ndani hutengeneza kiinitete cha mwanadamu.

Wakati huo wa kugawanyika, anasema Dkt. Anderson katika kitabu chake, Modern Ways to Health Vol. 2 (uk. 610), "chembe za ndani zinakuwa hazijaanza kujigawa katika vikundi kama vile chembe za neva, za figo au za misuli." Na hiyo ndiyo sababu kwanini hizo huitwa 'chembe za msingi' (stem cells). Chembe hizo ndizo hutengeneza karibu chembe nyingine zote mwilini.

Jarida, New Scientist, katika makala ya 'Stem Cells and the Future of Regenerative Medicine,' linasema hivi: "Miaka mitatu iliyopita (1999-2002), imewezekana kuondoa chembe za msingi za kiinitete kutoka katika kibonge cha chembe zinazogawanyika na kuzihifadhi zikiwa katika hali hiyo hiyo katika maabara."

Chembe za msingi za kiinitete zinaweza kustawishwa ili zitengeneze chembe nyingine nyingi za kiinitete. Chembe hizo zilitolewa katika mwili wa panya na kustawishwa mwaka 1981, zimezalisha mabilioni ya chembe nyingine za aina yake katika maabara.

Kwa kuwa chembe zote zilizohifadhiwa hubaki katika umbo lilelile, wanasayansi wanaona chembe hizo za msingi zikistawishwa katika mazingira yanayofaa ya kibaiolojia, zinaweza kutengeneza chembe zozote zile zinazohitajiwa katika matibabu ya kurekebisha tishu za mwili. Inadhaniwa kwamba chembe za msingi zinaweza kutumiwa kutibu viungo vingi vyenye matatizo ya kiafya.

Katika uchunguzi wa wanyama uliofanywa mara mbili, linaandika jarida, Science News, "watafiti walitumia chembe za msingi za kiinitete kutengeneza chembe zinazotengeneza insulini." Chembe hizo zilitiwa ndani ya mwili wa panya aliyekuwa na kisukari.

Uchunguzi mmoja ulionesha dalili za ugonjwa wa kisukari zilitoweka, na katika uchunguzi wa pili, chembe hizo mpya hazikuzalisha insulini ya kutosha. Katika uchunguzi mwingine kama huo, wanasayansi walifaulu kwa kiasi fulani kurekebisha kazi za neva za uti wa mgongo uliojeruhiwa, na kutibu ugonjwa wa kutetemeka.

Shirika la Taifa la Sayansi la Marekani, kwa mujibu wa jarida, Newsweek, linasema: "Uchunguzi huo unatoa matumaini, lakini hatuna uhakika iwapo matibabu kama hayo yanaweza kuwa na matokeo mazuri kwa wanadamu." Kwanini utafiti wa chembe za msingi za kiinitete unazusha ubishi?

Mzozo unatokea kwa sababu kiinitete hufa wakati chembe zake za msingi zinapochukuliwa. Limekariri Newsweek, Shirika la Taifa la Sayansi nchini Marekani linasema kufanya hivyo kunazuia kiinitete kukua inavyotakiwa mtu mzima.

"Wale wanaoamini kwamba uhai wa mwanadamu unaanza mara mimba inapotungwa, wanaona kwamba utafiti wa chembe za msingi za kiinitete unakiuka sheria zinazopinga kuharibu uhai wa mwanadamu, hata kama nia ni njema kiasi gani."

Maabara hupata wapi viinitete vinavyotolewa chembe za msingi? Jarida, New Scientist linasema vinatolewa katika hospitali zinazotungisha mimba nje ya tumbo la uzazi.

"Mayai yanatolewa na akina mama kwa kusudi hilo," likasema jarida, New Scientist na kuongeza, viinitete vinavyosalia hugandishwa au kutupwa. Hospitali moja ya India hutupa zaidi ya viinitete 1,000 vya watu kila mwaka.

Wakati utafiti wa chembe za msingi za kiinitete ukiendelea, watafiti baadhi wanakazia macho aina nyingine ya chembe ya msingi ambayo haizushi mzozo mkali. Chembe hiyo ni ya msingi ya tishu (adult stem cell).

Taasisi ya Taifa ya Afya ya Marekani (NIH), kwa mujibu wa jarida, Newsweek, inasema: "Chembe ya msingi ya tishu haina kazi maalumu inayopatikana katika tishu halisi kama katika uboho wa mifupa, damu na mishipa ya damu, ngozi, uti wa mgongo, ini, tumbo na kongosho."

Hapo awali, uchunguzi ulionesha chembe za msingi za tishu hazikuwa na uwezo mkubwa kama chembe za msingi za kiinitete. Lakini kitabu, Essentials of Physical Anthropology kinasema, "uchunguzi wa baadaye wa wanyama unaonesha,aina ya chembe za msingi za tishu zinaweza kutengeneza tishu tofauti kabisa na zile tishu za kwanza."

Chembe za msingi za tishu kutoka kwenye damu ya uboho wa mifupa, zinaweza kuendelea kujitengeneza upya katika uboho na kuzalisha chembe za damu za aina zote," anasema Dkt. Stanley Adams katika kitabu chake, There Are Such Things.

Tayari chembe hizo za msingi zimetumiwa kutibu saratani ya damu na matatizo mengine ya damu. Wanasayansi wengine wanadai chembe za msingi za tishu kutoka kwenye damu na uboho wa mifupa zinatengeneza chembe nyingine kama vile za ini na neva na chembe nyingine zinazopatikana kwenye ubongo.

Watafiti wa Marekani walipiga hatua muhimu sana kwa kutumia aina nyingine ya chembe za msingi kutoka kwenye uboho wa panya. Uchunguzi wao uliochapishwa katika jarida, Nature, ulionesha kwamba chembe hizo zinaweza kutumiwa kwa njia mbalimbali kama chembe za msingi za kiinitete.

Makala moja kwenye jarida, TIME inasema hivi: "Inadhaniwa kuwa chembe hizo za tishu zinaweza kufanya kazi zote za chembe za msingi za kiinitete." Lakini mafanikio ya wanasayansi hao ni baraka isiyokuwa na matatizo?

Watafiti waliochunguza chembe za msingi za tishu bado wanakabiliwa na matatizo makubwa. Kwanza, chembe hizo hazipatikani kwa urahisi na pili, ni vigumu kuzitambua hata zinapopatikana.

Faida moja kubwa, matumizi ya chembe hizo katika matibabu hayataangamiza viinitete vya binadamu. Ikiwa hivyo ndivyo, hilo linamaanisha matibabu yake hayawezi kudhuru afya ya mtu anayeyapokea?

Ukweli ni kwamba hata wanasayansi wakiboresha mbinu za kutengeneza tishu za kupachikwa mwilini, matibabu ya aina yoyote yanayotumia chembe za msingi bado yatakuwa na kasoro kubwa.

Tatizo moja kubwa ni kwamba mfumo wa kinga wa mgonjwa hukataa tishu mpya. Hivi sasa wanasayansi wanatatua tatizo hilo kwa kutumia dawa kali sana ambazo huudhibiti mfumo wa kinga, lakini dawa hizo huudhuru mwili.

Wanasayansi huenda wakabadili maumbile ya chembe za urithi, wakatatua tatizo hilo ikiwa wanaweza kubadili chembe za msingi ili tishu zinazostawishwa zisikataliwe na mwili wa mgonjwa.

Uwezekano mwingine ni kumtibu mgonjwa kwa chembe za msingi za tishu zake. Majaribio ya awali hospitalini yanaonesha, chembe za msingi zinazostawisha chembe zote za damu zilitumiwa kwa njia hiyo hiyo katika kutibu ugonjwa wa ngozi ujulikanao kama 'lupus'.

Ugonjwa wa kisukari unaodhibitiwa na insulini huenda ukatibiwa kwa njia hiyo, ikiwa tu tishu mpya haikataliwi na mfumo wa kinga na inaweza kukinza kile kilichosababisha ugonjwa huo.

Watu wanaougua magonjwa ya moyo, wanaweza kufaidika pia na matibabu ya chembe za msingi. Pendekezo ni chembe za msingi zitolewe mapema mwilini mwa watu walio katika hatari ya kupatwa na magonjwa ya moyo ili ziweze kustawishwa na kutumiwa baadaye ugonjwa unapozuka.

Ili kuondoa tatizo la tishu kukataliwa na mfumo wa kinga, wanasayansi wanapendekeza kumtengeneza mtu mwingine pacha kutokana na chembe za mgonjwa, kisha kumhifadhi tu akingali na kibonge cha chembe, ndipo wachukue chembe zake za kiinitete.

Tishu ambazo zingestawishwa na chembe hizo za msingi zingekuwa sawa na zile za mgonjwa, hivyo haziwezi kushambuliwa na mfumo wake wa kinga. Ingawa wengi wanaona kuwa mbinu hiyo haifai kimaadili, huenda pia wasiweze kutibu ugonjwa wa kurithi kwa kutumia mbinu hiyo.

Jarida, Newsweek liliwahi kuripoti hivi: "Ili wanasayansi wafaulu kutibu magonjwa kwa kurekebisha tishu ni lazima wajue jinsi ya kufanya mfumo wa kinga ukubali chembe zilizopachikwa mwilini." Hilo ni mojawapo ya matatizo magumu zaidi katika utafiti wa matibabu haya.

Upachikaji wa chembe za kiinitete mwilini, unaweza kusababisha uvimbe, hususan uvimbe unaojulikana kama 'teratoma' unaoweza kuwa na tishu mbalimbali kama vile ngozi, nywele, misuli, gegedu na mifupa.

Wakati wa kukua kwa mtu, chembe hugawanyika na kukua kwa njia ya asili kadiri ya chembe za urithi. Lakini ukuaji huo unaweza kuvurugwa wakati chembe za msingi zinapotolewa kwenye kiinitete, na kustawishwa nje ya tumbo la uzazi na baadaye kurudishwa kwenye mwili wa kiumbe aliye hai.

Jarida, New Scientist lililotajwa hapo juu, chini ya makala, 'Stem Cells and the Future of Regenerative Medicine,' linasema: "Kwa sababu ya kutojua kiwango cha ujuzi wa sasa, huenda watu wakakosea kudhania kwamba kutakuwa na matibabu mapya siku za usoni katika sehemu nyingi.

"Utafiti wa chembe za msingi bado uko katika hatua za kwanza, na kuna mambo mengi yasiyojulikana ambayo yanazuia kutekelezwa kwa matibabu mapya yanayotegemea chembe za msingi za tishu au chembe za msingi za kiinitete. Ni wazi kwamba mambo mengi hayajulikani.

Lakini wanasayansi watakapofanikiwa, itamaanisha, huo ndio mwisho wa matatizo yao na ulimwengu huu? Taarifa ya New Scientist inasema baadhi ya wanasayansi wanatarajia upinzani mkali sana iwapo matibabu hayo yatafanikiwa.

Licha ya sanyansi ya chembe za msingi, maendeleo makubwa ya tiba yamefanywa katika miaka ya karibuni. Kama tulivyoona, sehemu ya maendeleo hayo yanazusha maswali mengi, hasa yale yanayohusiana na maadili na uchumu.

Share it:

Health/Afya

home

Post A Comment:

0 comments: