MWENYEKITI wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Dioniz Malinzi,
atawaongoza Watanzania kumpokea mwanariadha, Alphonce Simbu,
anayetarajiwa kuwasili jijini Dar es Salaam leo akitokea jijini Rio de
Jeneiro, nchini Brazil alikoshiriki michezo ya Olimpiki.
Mwanariadha huyo anarejea nchini akiwa amefanikiwa kuipa heshima
kubwa Tanzania katika michezo ya Olimpiki upande wa mbio ndefu
(marathon), zilizofanyika Jumapili iliyopita kwa kushika nafasi ya tano.
Simbu alikimbia mbio za marathon akitumia muda wa saa 2:11:15, ikiwa
ni sekunde 11 nyuma ya mshindi wa nne, Ghirmay Ghebreslassie na kushika
nafasi hiyo ya juu ambayo haijawahi kushikwa na mwanariadha yeyote tangu
mwaka 980, licha ya kukosa medali.
Akizungumza na MTANZANIA jana Rais wa Shirikisho la Riadha Tanzania
(RT), Antony Mtaka, alisema Simbu atawasili saa 7:00 mchana katika
Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam kwa
ndege shirika la Afrika Kusini na kupokelewa kishujaa.
Aliwaomba Watanzania kujitokeza kwa wingi kumpokea shujaa huyo
aliyepeperusha vyema bendera ya taifa na kueleza kuwa wadau wanapaswa
kutambua kwamba Simbu na wanariadha wengine wanahitaji kusaidiwa ili
kupata tunachotarajia.
“Watu waamke sasa na kuiangalia riadha kwa namna ya kipekee, kwani RT
tunaamini kuwa kama wanariadha wetu watapata maandalizi ya kutosha
michezo ijayo tutapata medali,” alisema.
Wakati mwanariadha huyo akisubiriwa kwa hamu kubwa, tayari Kampuni ya
Simu Tanzania (TTCL) na MultiChoice (DStv) zimetangaza kuwa zitampatia
zawadi maalumu shujaa huyo kutokana na kuiwakilisha vyema nchi kwenye
michezo ya Olimpiki.
Mtaka pia aliliambia MTANZANIA kuwa, Simbu ameandaliwa hafla maalumu
ya chakula cha jioni kwa ajili ya kumpongeza itakayofanyika Jumapili
hii, jijini Dar es Salaam itakayoongozwa na Waziri wa Habari, Utamaduni,
Sanaa na Michezo, Nape Nnauye.
Rais huyo aliongeza kuwa RT inahitaji sapoti kubwa ya wadau katika
maandalizi ya mashindano mengine ya kimataifa yakiwemo ya Nyika
yatakayofanyika mwakani nchini Uganda na yale ya dunia yaliyopangwa
kufanyika jijini London, Uingereza.
Wakati huo huo, akizungumzia mafanikio ya mwanariadha huyo kwa upande
wa Serikali, Nape alisema Simbu anastahili pongezi maalumu kutokana na
kuipeperusha vyema bendera ya taifa katika mbio za marathon Olimpiki.
“Tukiendelea kuwa na utamaduni wa kutowapongeza wanamichezo wetu
tutakuwa tunafanya vibaya, kwani Simbu amefanya vizuri kwa taifa lake.
“Nawashauri wadau wa michezo nchini kwamba mbali na kutoa pongezi
binafsi kutokana na juhudi za Simbu, pia tufanye jambo la kuwapongeza
washiriki wote waliokwenda kushiriki michezo ya Olimpiki kwa kuthamini
mchango wa kila mmoja wao,” alisema Nape.
Waziri huyo pia alitoa wito kwa makampuni mbalimbali kujitokeza
kumtumia Simbu kama balozi kwenye nembo ya biashara au taasisi zao, ili
kumsaidia mwanariadha huyo kujiendeleza kimichezo na maisha yake kwa
ujumla.
Aidha, Nape alieleza kuwa kutokana na maisha duni ya wanamichezo,
Serikali imepanga kuunda kamati ya kufanya tathmini ya maisha ya jumla
ya wanamichezo na kubadili mfumo wa uendeshaji wa vyama vyao ili
kuongeza tija katika kazi zao.
Simbu atawasili nchini akiongozana na wanariadha wenzake, Saidi Makula na Fabiano Joseph, walioshiriki mbio ndefu.
Navigation
Post A Comment:
0 comments: