KUNA mambo ambayo najivunia daima. Mojawapo ni kuwa muumini wa lugha
ya kiswahili. Nimekuwa katika pilika za mara kwa mara kujitahidi
kujifunza zaidi lugha hiyo siku hadi siku.
Desemba mwaka 2006, nilipata mwaliko wa kuhudhuria mafunzo kwa vyombo
vya habari kuhusu mlundikano wa kemikali mbalimbali zilizoingizwa
barani Afrika na kutelekezwa huku zikileta madhara kwa wakazi wa bara
hilo. Kemikali hizo ni kama vile dawa za kuua wadudu katika mazao.
Waandaaji wa mafunzo hayo wakashinikiza kuwa waalikwa sharti
wajiandae kushiriki mijadala ambayo ingeendeshwa kwa lugha ya
kiingereza. Wakasema kama kungekuwa na mshiriki ambaye hakuwa tayari kwa
hilo basi atoe taarifa ili nafasi yake ichukuliwe na mtu mwingine.
Bahati nzuri ikawa upande wangu. Katika chumba changu cha habari
kulikuwa na waalikwa wengine. Kwa pamoja tukafanya kikao kujadili sharti
hilo. Tukajiuliza sababu za msingi za waandaaji kufanya hivyo.
Tulipowapigia simu kuwauliza mashiko ya sharti lao hawakuwa na sababu za
msingi. Washiriki wengi walikuwa Watanzania na Wakenya ambao kiswahili
ni sehemu ya maisha yao.
Nasi kwa upande tukasema kuwa tusingekuwa tayari kushiriki mafunzo
hayo kwa sharti la utumiaji wa Kiingereza. Kwamba kama mshiriki
angejisikia kutumia lugha hiyo ya kigeni basi afanye hivyo kwa ridhaa na
isiwe lazima. Mwishowe waandaaji wakanyosha mikono juu na kukubali hoja
yetu.
Yapo matukio mengi yafananayo na hayo. Semina mbalimbali
zimewalazimisha washiriki kutumia lugha ya kiingereza hata kama
washiriki wengi ni Watanzania wanaojua vema kiswahili. Wanabaki na pingu
zao kichwani. Pingu za utumwa wa akili zinazowafanya waendelee kuamini
kuwa matumizi ya kiingereza na sehemu ya kuonekana mpevu katika masuala
mbalimbali.
Hata watoto wa shule wanaozungumza kiingereza ni fahari kwa wazazi na
walezi wao. Kundi hilo la watoto huonekana kuwa ni la werevu kuliko
wanaozungumza kiswahili pekee. Wazazi wanasahau kuwa kukibeza kiswahili
na kukikumbatia kiingereza pekee ni hatari kwa taifa na utamaduni wake.
Sisemi kuwa Kiingereza kisifundishwe nchini. Hoja iliyo mbele yetu ni
umuhimu wa kukikumbatia Kiswahili ili kuendeleza utamaduni wetu.
Kuipuuza lugha hiyo ni dhambi ambayo wanaohusika wanapaswa kutubu.
Mara kadhaa natumbukia nyongo ninapowasikia baadhi ya wabunge
wakichangia mijadala mbalimbali ya Bunge kwa kutumia lugha ya
kiingereza. Unashangaa ni namna gani mbunge huyo anashindwa kutambua
kuwa yupo katika ardhi ya Tanzania na si kwa Malkia Elizabeth.
Wapigakura wake wengi hawaelewi hoja yake inalenga kitu gani. Mbona
wakati wa kampeni hatuwasikii mkitumia kiingereza? Wengi wenu
mnazungumza kiswahili mnapoomba kura. Tena wengine huenda mbali na hapo
na kuzungumza lugha za makabila yao. Hiyo ni hatua nzuri ya kuenzi mila
na utamaduni.
Itoshe basi kusema kuwa kama mlikuwa mmejisahau, huu ni wakati wa
kuamsha fikra zenu mpya na kukubali kuwa Kiswahili ni chetu na hatuna
budi kukikumbatia. Usipothamini cha kwako nani atakithamini? Husemwa
kuwa msahau kwao ni mtumwa.
Hivyo basi, huu ni wakati wa kujitambua na kukubali mema ya kwetu na
kuachana kabisa na utumwa wa akili ambao umedumu kwa miaka mingi sasa.
Navigation
Post A Comment:
0 comments: