WIKI hii imeanza vema kwa Tanzania kimichezo. Barani Ulaya, mshambuliaji Mbwana Samatta ameweka rekodi ya kuwa Mtanzania wa kwanza kuwa kinara wa upachikaji mabao katika mojawapo ya Ligi Kuu za bara hilo katika hatua za awali.
Samatta amefunga mabao matatu kwenye Ligi Kuu ya Ubelgiji kupitia klabu yake ya Genk; sawasawa na na Filip Markovic (Mouscron-Peruwelz) na Jeremy Perbet (Gent) wenye mabao matatu kila mmoja.
Kwa Samatta, kufunga kunakuja kama kunywa maji au kula chakula. Ni jambo la asili kwake kama historia yake katika soka inavyoonyesha.
Ameenda kujiunga na Genk akitokea TP Mazembe ya DR Congo, akiwa kama mfungaji bora kwenye michuano ya Klabu Bingwa Afrika msimu uliopita.
Alipokuwa na Kimbangulile FC ya kwao Mbagala, African Lyon na Simba amefunga sana mabao. Vipi umshangae Samatta leo?
Kufunga ni kama sehemu ya utaratibu wake wa maisha ya kila siku kuwa ataamka asubuhi, ataswaki, ataenda mazoezini, atarudi, atakoga, atakula kisha atapumzika. Ni kawaida yake.
Katika kiwango cha wanamichezo wa ndani Samatta, ameshapenya. Haitaji kushikiwa kalamu na kuandikwa mara kwa mara.
Mwishoni mwa wiki iliyopita kulikuwa na matukio makubwa mawili ya kimichezo nchini.
Mosi ni Mwanariadha wetu Alphonce Simbu, kushika nafasi ya 5 katika mbio za Marathon nchini Brazil, kwenye michuano ya Olimpiki.
Pili ni timu ya soka taifa ya vijana ya Tanzania ‘Serengeti Boys’, kuwatoa Afrika Kusini ‘Amajimbos’ na kujiweka katika nafasi nzuri ya kufuzu fainali za vijana nchini Madagascar mwakani.
Hivi ni vitu vya kupongeza, japo si vya kupongeza sana maana havijafikia lengo. Serengeti Boys, bado haijafuzu na Simbu hajashinda kitu zaidi ya kushika nafasi hiyo ambayo Tanzania, haijawahi kushika tangu mwaka 1964.
Serengeti Boys ya mwisho kufikia hatua hii na kuipita ilikuwa ya kocha Abdallah ‘King’ Kibadeni mwaka 2002, ambayo ilikuwa na nyota wengi wanaocheza hivi sasa na wengine kustahafu.
Tangu kutoka Serengeti Boys hiyo, hakuna Serengeti Boys nyingine iliyofikia hata robo ya mafanikio ya Serengeti Boys ya Kibadeni.
Serengeti Boys nyingi zilikuja na kuondoka, lakini hakukuwa na Serengeti Boys kama hii ambayo inaonyesha mwanga fulani mbele.
Si vibaya tukianzia hapa. Tuanzie kwa Simbu na Serengeti Boys hii ili miaka michache baadae tuje kuzungumza matunda ya mafanikio yetu kuanzia hapa.
Kwa Kimbu tuanze kutafuta nafasi za 1, 2,3, maana hivi sasa tunayo nafasi ya tano. Iko mikononi mwetu.
Alichokifanya hakitakuwa na maana kama katika michuano ya Olimpiki inayokuja Tokyo 2020, tutaenda kuipoteza nafasi hiyo na kukosa hata tatu bora au nafasi ya kwanza.
Haitakuwa na maana kama tukienda katika Olimpiki ya 2020, tukaanza kutafuta nafasi za 7, 8 au 10. Haitakuwa na maana.
Mwisho wa michuano ya Olimpiki ya sasa ndio mwanzo wa michuano ya Olimpiki nyingine. Huu ni usemi unaotumiwa na nchi mbalimbali zinazoshinda medali. Miaka minne kutoka sasa si mingi. Ni miaka michache sana kwenye suala la maandalizi.
Kama nchi tumeshindwa kujipanga vyema kuanzia kwa wakimbiaji wa zamani Selemani Nyambui (1980), Filbert Bayi (1974), si vibaya tukianzia hapa kwa Simbu.
Itahuzunisha kama miaka kadhaa tukikutana tena hapa kumzungumza Simbu, kuwa aliwahi kushika nafasi ya tano katika mbio za Marathon 2016, Rio nchini Brazil, huku tukishindwa kuzalisha wakimbiaji wengine watakaoipeperusha vyema bendera yetu kimataifa.
Dunia ya leo michezo ni ajira. Michezo ya leo si sehemu ya kuweka miili katika hali nzuri tena.
Kama wakina Bayi, Nyambui, walishinda medali muda ambao michezo ilikuwa ya kujitolea tunashindwaje kuandaa vijana ambao watakuja kuipa mafanikio nchi na wao wenyewe?
Ni wakati wa Waziri wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Nape Nnauye na Rais wa Riadha nchini Anthony Mtaka ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa Simiyu, kutazama upya suala la fursa zilizoko michezoni.
Tusidanganyane. Hakuna nchi au mwanamichezo aliyefanikiwa bila mkono wa serikali nyuma yake.
Hata leo hii serikali kama ikiamua Tanzania, ishiriki michuano ya Kombe la Dunia mwaka 20
Post A Comment:
0 comments: