‘Watoto bandia’ washindwa kuzuia mimba za mapema

Share it:
Mradi unaolenga kupunguza idadi ya wasichana wanaopata mimba mapema kwa kutumia watoto bandia nchini Australia, huenda umesababisha matokeo ambayo hayakuwa yanatarajiwa ama ambayo hayakutakikana.
Chini ya mpango huo kwa jina Virtual Infant Parenting Programme, zaidi ya wasichana 1,000, walitakiwa kutunza watoto bandia ambao walikuwa wakipiga kelele, kulia na kutoa sauti za kunyongwa na chakula.
Lengo lilikuwa kuwazuia kupata mimba ya mapema na kuwafanya kuelewa usumbufu na matatizo ambayo watu hukumbana nayo wakiwalea watoto.
Washiriki wa mpango huo uliotekelezwa magharibi mwa Australia pia walipewa mafunzo ya afya ya uzazi.
Baadaye ilibainika kwamba walipotimiza umri wa miaka 20, wasichana walioshiriki katika mradi huo, walikuwa na uwezekano mara dufu wa kupata mimba ya mapema kuliko wale ambao hawakushiriki katika utafiti huo.



Uchunguzi uliofanywa baada ya wasichana hao kutimiza miaka 20 ulibaini kwamba asilimia 8 wakati huo walikuwa wamejifungua angalau mara moja na asilimia 9 walikuwa wametoa mimba.
Matokeo ya utafiti huo yamechapishwa katika jarida la kimatibabu la Lancet.
Watafiti wanasema baadhi ya sababu ambazo huenda zilifanya mradi huo kutofanikiwa ni kwamba haukuangazia wavulana, ambao pia huchangia katika wasichana kushika mimba.
Aidha, huenda watafiti walichelewa kuanza kuwafunza wasichana waliokuwa tayari wamejiunga na shule za upili.
Aidha, wanasema watoto bandia hawawezi wakaonyesha kwa njia halisi taswira ya kumtunza mtoto halisi.


Share it:

Habari zilizosomwa zaidi

Post A Comment:

0 comments: